25 November 2010

kampeni za udini katika siasa za tz

Tutegemee vyama vya kianglikana na kianswar sunna uchaguzi ujao  
                      Mussa Juma

IMEKUWA ni kawaida kila wakati wa uchaguzi kuibuliwa hisia za kidini miongoni mwa vyama vya siasa na wagombea.
 
Hisia hizo za kidini,  zimekuwa zikitumiwa kama mtaji wa vyama pale  ambapo chama kimoja kitakapotuhumiwa ni cha kidini.
 
Kwa bahati mbaya sana propaganda za siasa za kidini zimekuwa zikitumiwa kudhoofisha vyama vya upinzani hasa pale  chama  kimoja  kinapoonekana kuwa na nguvu.
 
Dhana ya udini ilianza kupamba moto katika chaguzi za mwaka 2005 pale  ilipotumika  kukidhoofisha  chama cha  wananchi CUF  baada ya kukituhumu kuwa ni cha kiislam.
 
Katika uchaguzi wa mwaka huu, tuhuma zile zile zilizopunguza nguvu ya CUF, zimehamia chadema na sasa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kidini wamesikika wakikihusisha chama hicho na kikristo.
 
Bila aibu wala hofu ya kutumia siasa za dini kuwagawa watanzania, baadhi viongozi katika uchaguzi wa mwaka huu, wameweza kutumia dhana hiyo ya udini kwa mafanikio japo si yale yaliyokusudiwa.
 
Katika siasa hizi za kidini, kwa bahati mbaya zaidi baadhi ya viongozi wa dini  wamekuwa wakijikuta wakiingizwa kuzishabikia bila hata wao kufanya tafiti na kujua athari za matamko yao .
 
Ingawa viongozi hawa wa dini, wanamapenzi na vyama vya siasa lakini baadhi wameshindwa kufisha hisia zao na kuchotwa na wanasiasa na hivyo kutumika kama vipaza sauti vya vyama fulani.
 
Mara nyingi imetokea  baadhi ya viongozi wa dini, kujikuta wakiwa washabiki wa chama tawala na kutoa matamko tata yasiyo ya kidemokrasia  na hapo hupongezwa na hakuna ambaye hutamka kuwakosea viongozi hao.
 
Katika uchaguzi wa mwaka 2005, kuna baadhi ya viongozi wa dini walipaza sauti zao na kutamka kuwa,aliyekuwa mgombea wa CCM wa Urais wa chama tawala ni chaguo la mungu.
 
Waliopaza sauti hizo walipongezwa kila kona na hakuna ambaye aliwaonya kuwa wanaeneza siasa za kidini.
Wengine walitumia madhabahu yao , kukituhumu chama cha CUF wakati huo ni cha kidini na kuwasihi watanzania kuwa makini na  chama hicho.
 
Hata hivyo, kila baya lina uzuri wake, kuhusisha chama na dini Fulani kumesaidia vyama hivyo kupata wanachama ambao ni watiifu wa dini zinahohusishwa na chama.
 
Hili lipo wazi tangu ipazwe sauti kuwa  CUF ni chama cha waislam kimesaidia maeneo yenye waislam wengi kukiunga mkono chama hicho na hili lipo wazi.
 
Na katika uchaguzi wa mwaka huu, pale chadema walipohusisha na ni ya kikristo kuna maeneo mengi, kumesaidia wakristo kukipigia kura chama hicho na hata kutwaa majimbo muhimu kama Arusha mjini.

Sidhani kama walivumisha sauti hizi za udini, wamejifunza katika hilo japo kuwa sasa chama cha udini cha mwaka 2005 kimeunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar .
 
Hata hivyo, wakati vyama vya CUF na Chadema vikihusisha na dini chama tawala kimekuwa  kisafi hakina dini ni cha kipagani na ni cha wote, lakini je matamko haya yana manufaa.
 
Kama tukiachia hili tusishangae chaguzi zijazo kuna vyama vitaingizwa katika madhehebu fulani kwani dini mbili tayari zimetumika,  sauti zitapazwa chama hiki ni cha   Kiangilikana na hiki ni cha Answar Sunna  na hapo tutakuwa tumefika pabaya zaidi.
 
Tukifikishwa katika siasa za madhehebu  watatueleza kuwa  dhehebu hili linakubali matendo haya na hili ni lazima ufanye matendo haya na hapo tutakuwa tumekwisha watanzania.
 
 Nionavyo mimi kwa ujumla wake kuhusisha chama na dini fulani ni jambo la hatari sana na athari zake ni kubwa kama  na  vurugu za kidini historia zinaonesha zimekuwa hazidhibitiki tutazame Israel na Palestina na hata tutazame yanayofukuta Sudan na nchi nyingine za Ulaya.
 
 
Binafsi sihusishi chama chochote na dini yoyote kwani kihistoria katika mapambano yoyote lazima kupata kwanza wafuasi wa kundi fulani ambao watakuunga mkono zaidi na kuungwa mkono huko hakuna maana ndio msingi wa chama au wapiganaji wote.
 
Wakati wa kudai uhuru historia inaeleza wazi kuwa Waislam wa jijini Dar es Salaam na Pwani walimuunga sana mkono sana hayati Baba wa Taifa mwalimu Julias Nyerere  katika harakati za kudai uhuru .
 
Baadhi ya Waislam wa Dar  es salam walifikia hatua ya kumuingiza msikini hayati Nyerere ,kumchagia sadaka na  kufunga kwa ajili yake na hata kumtaka  yeye kufunga na hata walimfanyia swala maalum.
 
Lakini hakuna ambaye alihusisha chama cha  TANU kuwa ni chama cha kiislam, japo kuwa wafuasi wake wengi wakati huo hata wale waliokuwa wakimuwezesha Mwalim Nyerere walikuwa waislam.
 
Hivyo hata sasa binafsi siwezi kusema chama chochote ni cha kidini hivi vyama ni vya watu wenye dini zao, imani tofauti lakini wanamawazo yanayofanana na mitazamo inayofanana katika kufikia malengo ya kushika dola.

Kwa msingi huu hiyo nina matatizo makubwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na kidini ambao katika karne hii ya 21 wanataka kuturejesha katika mawazo na mitizano mgando kwa kuhusisha dini na vyama vya siasa vilivyopo sasa.
 
Naamini viongozi hawa wanaotulazimisha tuanze kumwamini mtu kwa kupitia dini yake wamefilisika kimawazo na wamekosa jipya la kuwaridhisha watanzania waliowengi ambao maisha yao ni magumu.
 
Hivyo ushauri wangu ni kwa viongozi wetu wa kisiasa na kidini waache kuzitumia dini kwa maslahi yao , nawasihi sana waache mifumo ya kidemorasia ifanye kazi na hivyo tupate viongozi wiliobora na sio bora viongozi.
 
Mussa juma ni mwandishi   Arusha anapatikana simu 0715 296503, email mussa_juma@yahoo.com,mussanews.blogspoti.com.
 mwisho

No comments:

Post a Comment