20 September 2012

 Maajabu ya Asili ya Dunia ya Serengeti
.Maelfu ya nyumbu  kurejea  Serengeti kwa kuvuka mto  wa Mamba
                                    Mussa Juma.

HIFADHI ya Taifa ya Serengeti, ni moja ya maajabu saba ya asili ya duniani na miongoni mwa  mambo yanayosababisha uwepo  wa maajabu hayo ni mzunguko  wa maelfu ya wanyama aina ya Nyumbu kuhama hifadhi hiyo na kuhamia hifadhi ya Masai Mara na baadaye kurejea Serengeti kwa kupita katika mto Mara.
Watalii toka Mataifa mbali mbali duniani, wamekuwa wakifuatilia tukio hili ambalo halipatikani mahala popote duniani, kila mwaka ,pale Nyumbu hao wanaofikia ya 1.5 milioni, wakiwa wanaandama na wanyama wengine wakivuka mto na kurejea Serengeti.
 Tukio la kurejea Nyumbu hao Serengeti, linatajwa kuwa ni moja ya maajabu ya asili  saba ya dunia kwani Nyumbu hao,kwani  Nyumbu hulazimika kuvuka Mto Mara ambao umejaa maji na baadhi yao hufa kwa kuzidiwa na nguvu kubwa ya maji huku, wengine wakiliwa na  Mamba waliopo katika mto huo.
Kwa watalii ambao hufuatilia tukio hilo, hulazimika kutumia kati ya siku mbili hadi tano,ili kujionea makundi ya Nyumbu, yakivuka mto Mara katika njia mbali mbali safari ambayo huchukuwa takriban dakika 30 kwa nyumba kuweza kuvuka kama asipokamatwa na Mamba.
Tukio hili kwa upande wa wanyama walao nyama, hasa Mamba hugeuka ni sherehe kubwa kwao kwani, mawindo yao  huwa rahisi sana hasa kutokana na idadi kubwa Nyumbu, bila kujali kina cha maji na kasi yake, wanapokuwa wakivuka mto huo ambao kwa Mamba ni makazi yao.
Kabla ya Nyumbu hao, kuvuka sauti zao hutawaka kingo za mto, huku wakijikusanya makundi kwa makundi ili kuvuka na mmoja anapoanza kukanyanga maji  tu ili kuvuka mto, basi kundi zima humfuata bila kujali hatari iliyopo mbele yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanaoshuhudia tukio hilo la kipekee duniani hivi karibuni, ambalo mwaka huu, limeanza mwezi septemba tofauti na miaka mingine linapoanza mwezi octoba, Afisa Utalii wa hifadhi ya Serengeti,Seth Joseph Mihayo na Meneja Mahusiano wa Shirika la hifadhi za taifa(TANAPA), Pascal Shelutete na watalii toka ndani na nje ya nchi, walisema tukio la kurejea Nyumbu  ni la kipekee duniani na hutokea kila mwaka.
Mihayo anasema Nyumbu wanaofikia 1.5 milioni, huwa katika mzunguko katika hifadhi ya Serengeti na kusini mwa hifadhi katika mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na eneo la magharibi mwa hifadhi kila mwaka na  kuanzia Agosti huondoka katika hifadhi ya Serengeti na kwenda hifadhi ya Masai mara na hukaa huko kwa takriban mwezi mmoja kabla ya kurejea Serengeti.
“tukio hili  ambalo ni kati ya maajabu saba ya asili ya dunia yanayopatikana hapa Serengeti ni la aina yake kwani mara baada ya Nyumbu hawa wanapoingia Tanzania, husambaa  katika hifadhi ya Serengeti, Ngorongoro na maeneo ya magharibi mwa hifadhi ambapo huzaliana na baadaye kwenda Masai Mara tena ”anasema Mihayo.
Anasema mzunguko wa wanyama hao, ambao unafaida kubwa katika eneo zima la kiikolojia la Serengeti, umekuwa pia ni kivutio kikubwa cha watalii wa ndani ya nje ya chi.
“kinachovutia zaidi ni jinsi Nyumbu hawa wanapovuka  mto Mara bila kujali mwendo kasi ya maji, kina cha mto na hatari ya kulia na wanyama kama Mamba ambao katika kipindi hiki hujiandaa kwa chakula cha uhakika”anasema Mihayo.
                                                TANAPA kuwa na mapokezi ya Nyumbu Tanzania kila Mwaka
Meneja Mahusiano wa TANAPA, Pascal Shelutete anasema kuanzia mwaka huu, TANAPA imeamua kuwa na mapokezi ya Nyumbu hao hasa kwa kulitangaza tukio hili ndani na nje ya nchi.
“wenzetu tukio la Nyumbu kwenda kwao mwezi mmoja tu, hufanywa na kimataifa na sisi sasa ambao ndio huwatunza kwa muda mrefu Nyumbu hawa, tumeanza mpango wa kuwa na siku maalum ya kuwapokea wanaporejea nyumbani kutoka katika mapumziko”anasema Shelutete.
Anasema tukio hilo la maelfu ya Nyumbu kurejea Serengeti ingawa bado watanzania wengi hawajalishuhudia ni la aina yake na linaonesha uhalisia wa hifadhi ya Serengeti na upekee wa hifadhi hiyo Duniani.
“napenda kutumia fursa hii, kuwaomba watanzania, wajitokeze kila mwaka kutembelea Serengeti na kujionea maajabu haya ya asili na nina uhakika hawatajutia muda wao na gharama ndogo ambazo watapaswa kulipia”anasema Shelutete.
                                             Watalii wa nje wakisha wakisubiri tukio hili.
Tukio la kurejea Nyumbu, Serengeti hufuatiliwa na idadi kubwa ya watalii duniani, ikiwepo pia makampuni makubwa ambayo hujihusisha na upigaji picha za wanyama na masuala ya historia ya dunia.
Miongoni mwa watalii ambao walikuwa na mwandishi wa makala hii, wakisubiri kulishuhudia tukio hili ni, Truby Wivbenga na Mumewe Jan Wivbenga, toka nchini Uholanzi ambao walilazimika kukaa ndani ya hifadhi ya Serengeti takriba siku tano  wakisubiri tukio la nyumbu kuvuka mto Mara na kuingia Serengeti.
Truby anasema kabla ya kuja nchini, waliomba kampuni ya uwakala wa utalii ya Leopard kuwapangia siku kadhaa za kushuhudia tukio hilo la kipekee duniani na wamefarijika sana baada ya kujionea wenyewe maelfu ya nyumbu hao wakivuka mto na kuingia Serengeti.
“sasa tunarejea Uholanzi tumefurahi sana hili ni tukio kubwa katika historia ya maisha yetu , tutakwenda kulielezea kwetu tukifika, Tanzania mna bahati kubwa ya kuwa na tukio la aina hii”anasema Truby.
                                   Je ni kwanini Nyumbu usafiri hadi nchini Kenya kila mwaka.
Safari ya Nyumbu hawa,kutembea umbali wa takriban kilomita 100 kila mwaka wakitoka maeneo mbali mbali ya hifadhi na kwenda hadi hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya imekuwa ikizua maswali mengi lakini wahifadhi wanaelezea,
Mihayo anasema kubwa ambalo huwafanya Nyumbu hawa, kusafiri hadi nchini Kenya, ni kufuata Mvua na majani kwani mwezi Agosti katika hifadhi ya Serengeti na maeneo mengine ya jirani huwa kuna ukame  na hivyo malisho ya wanyama hawa ambao ni wengi katika hifadhi hiyo hupungua.
Hivyo licha ya hatari ya kuvuka mto na kuliwa na wanyama wengine, Nyumbu hulazimika kwenda Masai Mara kwa takriban mwezi mmoja na mara tu mvua zinapoanza kunyesha ukanda wa Serengeti basi huanza kurejea taratibu na kuvuka Mto Mara ambao wakati huo huwa tayari umejaa maji.
Anasema Msafara ya maelfu ya Nyumbu hawa, huchukuwa takriban mwezi mmoja hadi kukamilika na tukio hili licha ya kuwa kivutio kikuu cha utalii wa Serengeti pia lina manufaa kwa wanyaama wengine walau nyama na nyasi na pia hufuatiliwa na mashirika  na taasisi mbali mbali za kimataifa za utalii duniani na hivyo kulifanya eneo tukio hili kuwa la aina yake duniani.
Mussa Juma ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Mkoa wa Arusha anapatikana Email:mussa23@rocketmail.com au simu 0754296503.
MWISHO.



---

No comments:

Post a Comment