03 December 2010

baraza la mawaziri la maridhiano ndani ya CCM lina jipya

Tutegemee nini  Baraza la mawaziri la maridhiano ndani ya CCM.

                                    Mussa Juma.

MAWAZIRI  50 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , wameapishwa ,huku kukiwa na sura mpya 24 na sura zilizozoeleka ndani ya baraza hilo 26.

Uteuzi huu ambao umefanywa na Rais Jakaya Kiwete, umepokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbali mbali wa masuala ya siasa, wapo walipongeza, wapo walioomba mawaziri kupewa muda na wapo ambao wanaamini baraza hili ni vigumu kutekeleza Ilani ya uchaguzi wa CCM.

Wanaotilia shaka baraza hili, wanahoja mbali mbali kwanza wanaona bado ni kubwa,pili sura nyingi ni zile zile na pia ahadi za CCM zilikuwa nyingi sana katika uchaguzi uliopita hivyo kutekeleza zote ni ndoto ya mchana.

Lakini kikubwa zaidi katika baraza hili ni kuonekana  ni baraza la maridhiano ndani ya CCM kutokana na mawaziri wengi ambao hawakuwa wanamtando kupewa nafasi  katika wizara zenye majukumu makubwa.

Uteuzi wa baadhi ya mawaziri  na kupewa wizara kubwa nje ya mtandao  pia umepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wa masuala ya siasa.

 Wapo wadau   ambao sasa wanaamini Rais Kikwete kaamua kuweka kanda wapiganaji makubwa wa mtandao uliosaidia ushindi wake mwaka 2005  na wapo wanaoamini sasa ameamua   kuzima manunguniko ya baadhi ya wanasiasa wakongwe na  Wananchi kuhusu uteuzi ambao amekuwa akiufanya.

Baadhi ya Mawaziri ambao wanaaminika hawakuwa katika mtandao na sasa wapo katika wizara nyeti ni kama John Magufuli,ambaye ni Waziri wa Ujenzi, George Mkuchika waziri wa TAMISEMI,Dk Harryson Mwakyembe Naibu Waziri ujenzi,Shamsi Vuai Nahodha waziri mambo ya ndani,Lazaro Nyarandu Naibu waziri wa Viwanda na biashara na wengine kadhaa.

Ingawa kuna mawaziri wengine hawakuwa katika mtandao hata katika baraza lililopita na sasa wamerejeshwa katika uwaziri na kupewa wizara kubwa, kama Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Maji, kuteuliwa kwao kuna ishara kubwa ya muafaka ndani ya CCM.

Ni kweli usiofichika kuwa kuna baadhi ya mawaziri katika baraza lililopita waliokuwa wanamtandao na wengine hawakuwa wanamtandao, walionekana kupwaya sana katika nafasi zao na hata kufikia hatua ya kukosa mvuto katika jamii.

Lakini sasa baraza hili, kuna mawaziri  na manaibu wao kadhaa ambazo hawakuathiriwa  sana na mtandao na siasa za makundi ndani ya CCM na hivyo kutoa tumaini jipya  la kuona baraza la mawaziri linafanyakazi kwa pamoja na kwa ufanisi mkubwa.

Ninanavyo mimi baraza hili la maridhiano ndani ya CCM, linaweza kuwa na mafanikio makubwa kama wote walioteuliwa wakiamua kufanya kazi kwa maslahi ya Umma na kujitenga na siasa za makundi ya awali.

Na pia baraza hili, linaweza kumsononesha Rais Kikwete kama aliyowateua wakiendeleza makundi yao na hivyo kuhujumiana wao kwa wao.

Makundi  ndani ya CCM yamekipa chama hicho, msukosuko mkubwa kuanzia ndani ya chama hadi katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata kusababisha bunge la tisa chini ya aliyekuwa Spika, Samweli Sitta kufikia maamuzi mazito ya kihistoria.


Kwa upande mmoja migongano wa wakubwa hawa ndani ya CCM imekuwa na manufaa   kwa wananchi na upande mwingine pia umekuwa na athari kwa wananchi hasa pale miradi muhimu ya kijamii inapotelekezwa kwa kuzingatia tu aliyeasisi hayupo katika kundi Fulani.

Katika mazingira ya sasa kwa baraza hili, wengi hawatarajii tena kuibuliwa mambo mazito ambayo yanaweza kuitikisa serikali ya Rais Kikwete, hii inatokana na   muundo wa baraza hili.

Baraza  hili linaweza kurejesha nguvu ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 au kukimaliza chama hicho, hasa pale mawaziri hawa na wabunge wote wa CCM watakapoamua kusimama kidete na kutetea maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya umma.

Uteuzi huu pia unaweza ukawa mwisho wa umaarufu wa waliokuwa wabunge wapiganaji dhidi ya ufisadi kama, Waziri wa Afrika ya Mashariki, Samweli Sitta na Naibu waziri wa Ujenzi Dk Harryson Mwakyembe. kama watakuwa kimya kuzungumza hata   yale mambo   waliyoyasimamia na kuyapinga katika bunge lililopita.

Hata  hivyo, bado ni imani ya wengi kuwa, mawaziri hawa 50 licha ya kuwa mawaziri watatetea maslahi ya umma kwa nguvu zao zote na kujitenga na kutumia nafasi zao kwa manufaa yao .

 Mawaziri hawa, wananafasi kubwa  ya kubadilisha historia ya taifa hili, pale watakaporuhusu mijada muhimu bungeni na kutoa majibu yenye tija katika masuala ya msingi yanayolalamikiwa  na watanzania.

Miongoni mwa mambo hayo ni kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao, kuhakikisha Tanzania inakuwa na katiba mpya na pia kuhakikisha vita dhidi ya vitendo vya Rushwa na ufisadi, madawa ya kulevya, matumizi mabaya ya madaraka vinapiganwa kwa dhati na sio kwa maneno matupu.

Lakini kama baraza hili,litarejea kule tulipotoka katika siasa za makundi,siasa za kutetea maslahi binafsi, siasa za kuchafuana ni wazi  matarajio ya walio wengi yatakuwa yametoweka na baraza hili halitakuwa  tena baraza la maridhiano ndani ya CCM bali litaongeza mpasuko.

mussa juma ni mwandishi wa mwananchi mkoa wa Arusha, anapatikana  0754296503 email mussa_juma@yahoo.com,mussanews.blogspot.com

MWISHO.


No comments:

Post a Comment