03 December 2010

Wanahabari na vita dhidi ya UKIMWI.

WAANDISHI wa habari nchini, wameombwa kujiepusha na vitendo hatarishi ambavyo vinachangia maambukizi dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Mbunge wa Jimbo la Arusha,Godbless Lema, alitoa wito juzi  wakati akifungua semina ya siku moja ya waandishi wa habari mkoani Arusha juu ya masuala ya UKIMWI ambayo ilifanyika Ricks Morden klabu .


Lema alisema waandishi wa habari kama wanajamii wengine, wanakabiliwa na tishio kubwa la maambukizi ya UKIMWI kutokana na mazingira ya kazi zao.

“nawapongeza  waratibu wa semina hii na mimi kama mbunge nawahakikishia tutaendelea kushirikiana wakati wote kama masuala haya ya kijamii”alisema Lema.

Akitoa mada katika semina hiyo,Dk Saimon Megiroo  toka hospitali ya Selian mkoani hapa, alisema wanahabari ni wadau muhimu sana katika vita dhidi ya Ukimwi kama wakitumia kalamu zao kuelimisha vyema jamii.

“Selian tuna kitengo cha masuala ya Ukimwi na moja ya wadau wetu katika masuala ya uelimishaji ni wanahabari”alisema Dk Migiroo.

Naye Meneja mahusiano ya shirika la mtandao wa wafugaji PINGOS Forum Stivin Shikuku akitoa mada katika semina hiyo, alisema  jamii za wafugaji  bado zinaathirika sana na ukimwi kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha.

Akitoa mada juu ya tafiti za vita dhidi ya UKIMWI katika jamii hizo, alisema bado huduma muhimu  za  afya kama upimaji na upatikanaji wa dawa za kurufusha maisha katika jamii hizo  hazipatikani.

Awali Meneja wa shirika la PSI mkoa wa Arusha na Manyara, Chris Mbajo akitoa mada yake juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI aliwataka wanahabari kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vitakavyo wafanya wapate maambukizi.

Semina hiyo ya wanahabari iliyodhaminiwa na mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, shirika la wafugaji la Pingos Forum, iliandaliwa na chama cha waandishi wa michezo mkoa Arusha(TASWA) kwa ushirikiano na kampuni ya Ms Unique na chama cha wanaoishi na virusi cha Tumaini Positive(TUPO).
MWISHO.

No comments:

Post a Comment